SONONA/KUSHUKA MOYO

SONONA (DEPRESSION) SI HISIA TU.
By Bernadether Bwire

" Depression is a prison where you are both a prisoner and a cruel jailer." ~Anushka Sharma

"... It's like someone turned off the light inside my head...Like always the world around me loses focus and I'm trying to make sense out of it". ~Shaheen Bhatt.

Katika maisha kuna nyakati binadamu tunapitia ambapo tunahisi, kuiona na kuifikiria Dunia kama giza nene. Kutokuona muelekeo wa maisha, kutokuhisi hamu ya kufanya chochote na pia kuona hakuna maana ya kuendelea kuishi duniani. Katika nyakati hizi mtu hutawaliwa na mawazo hasi ambayo yakizidi huweza mfanya mtu ajiue. Mawazo hayo hasi huongeza kudhoofika kwa moyo kwani mawazo au fikra hujawa mambo mabaya tu yaliyomtokea mtu, yanayomtokea na pia yatakayomtokea mtu. Mara nyingine si kweli kwamba mtu hukutwa na mambo haya mabaya bali katika nyakati hizi akili ya utambuzi huzibwa na mawazo hasi hivyo kusababisha mtu ashindwe kabisa kuona mwanga katika maisha yake. Kuna baadhi yetu ambao huchukulia hali hii ni ya kawaida na ya kujitakia  na huwaona wahanga kama watu wanaofanya kusudi na kujitegeza. Sonona ni tishio kubwa sana katika maisha yetu na imeondoka na maisha  ya watu wengi sana na bado imewafanya watu baadhi kuwa walemavu wasioweza kufanya kazi zao za kila siku vizuri. Pia shirika la Afya Duniani linatabiri kuwa Sonona isipotiliwa manani inakuja kuwa tishio kubwa sana ulimwenguni katika kuleta maendeleo endelevu. Basi kwa kushirikiana sote tukumbushane kuwa Sonona si yakujiendekeza, kujitakia ama kujitegeza na ni ugonjwa kama magonjwa mengine. Pia tunatakiwa tukumbushane kuwa matibabu ya sonona yanahitaji muda na mgonjwa wa sonona akitibiwa huwa raia mwajibikaji na wa muhimu kama raia wengine.

Kraepelin alisema: " Saa nyingine hisia hutawaliwa na kujishusha nafsi kusikokwisha na hujawa giza nene linaloashiria kutokuwepo kwa matumaini. Mara nyingine maradhi ya wasiwasi yanayoonesha kutokufikia mwisho. Moyo wa mgonjwa huwa mzito sana na hakuna kitu kinachoweza kumpa raha. Hujihisi mpweke, mwenye huzuni isiyoelezeka kama kiumbe aliyenyang'anywa urithi wa hatma yake nzuri; mgonjwa huwa na wasiwasi na uwepo wa Mungu na hujisalimisha katika hisia na fikra za kupoteza hamu ya kufanya chochote inayofunga na kuziba kila kitu kizuri maishani mwake, pia kuzima mwanga wote unaomulika maisha yake. Kila kitu kinaanza kupingana na yeye; na kila kitu kinazidi kumuumiza na kumdhoofisha  sana.... Kila sehemu akiangalia huona giza nene pamoja na ugumu wa maisha; watu waliomzunguka anaanza kuwaona hawajali na hawana huruma Kama alivyodhani mwanzo.... Maisha kwa mtu huyu huonekana hayana maana Wala thamani." (   Hammen, 1997)

" ...kuongea ilikua ni tabu sana, kulala ilikua ni shida kwangu, kila kitu nilihisi kimenielemea. Kufikiri ndio ilikua kitu kigumu sana kwangu kipindi hicho....Kwenda kukutana na daktari na kugundua mtazamo wa kiafya ilikuwa ni mzigo sana kwangu kwani hata mimi nilikuwa ninamtazamo wangu kuhusu hali hii. Kuna fikra zilinijia kwamba hali hii ni matokeo ya makosa yangu niliyoyafanya kipindi cha nyuma. Kwa kweli ni hatari sana kupitia hali au hatua pale nafsi yako inajishusha thamani".~ Angelo (WHO).

"Ninaposhuka moyo ninakosa hamu ya kufanya chochote, hata mambo ambayo kwa kawaida huwa napenda kufanya. Kitu pekee ninachotaka ni kulala. Mara nyingi ninahisi kuwa watu hawanipendi, sina thamani na mimi ni mzigo kwa wengine. Kushuka moyo ni kama kufungiwa kwenye shimo kubwa lenye giza na lisilokuwa na mlango mkubwa wa kutokea. Unahisi kama unarukwa na akili, na kwamba umebadilika kabisa tofauti na ulivyokuwa zamani."~Anna ( JW, Amkeni! 2017).

"Nilifikiri kujiua. Kusema kweli sikutaka kufa. Nilitaka tu kuepuka hisia mbaya nilizokuwa nazo. Kwa kawaida mimi ni mwenye kujali sana, lakini ninaposhuka moyo, sijali yoyote Wala kitu chochote." ~Julia ( JW, Amkeni!, 2017) 

Shirika la Afya duniani WHO katika kuazimisha siku ya Afya duniani mwezi wa nne, mwaka 2017, lilichagua kuweka wazi kuhusu matatizo ya akili kama kizuizi katika maendeleo endelevu na amani Duniani. Huku wakichagua Sonona au Kushuka moyo ( depression)  kama mada ambayo inagusa kila sehemu na kila nchi. Na pia walichagua Sonona kwasababu ni chanzo kinachoongoza katika kupelekea ulemavu Dunia mzima na pia ni chanzo kikuu cha magonjwa.

Kauli mbiu katika mkutano huo ilikua ni " Let's talk". Ikiwalenga wahanga wote wa Kushuka moyo au sonona kutokukaa kimya kuhusu yanayowasibu bali kufunguka kuhusu hali hiyo kwa watu wao wa karibu wanaowaamini iwe baba, mama, rafiki au daktari. Kufunguka huku na kuongea ni hatua moja katika kuishinda hali hii. Sonona ni nini hasa? Nini chanzo?. Dalili zake ni zipi? Na kwanini ni janga la Dunia na linatakiwa litiliwe mkazo kama lilivyotamkwa na WHO. Kwa hii makala tutaangilia vitu viwili tu kwanza ambavyo ni maana ya sonona n viashiria vyake.

 Sonona ni nini?

Sonona ni muunganiko wa kihisia, kimwili/kifizikia, kiutambuzi na kitabia ambapo vyote hivi hudhoofika sana na kuharibika utendaji wake wa kazi au kudumaa kwa kipindi cha muda mrefu.
Udhoofikaji au uharibikaji wa utendaji kazi wa muunganiko wa hivi vitu ndio uashiria kwamba mtu huyu anasumbuliwa na sonona (depression). ( Hammen, 1997)

Sonona sio msongo wa Mawazo ( stress) lakinj msongo wa mawazo uliopitiliza na kudumu muda mrefu unaweza sababisha sonona. Sonona hii tunayoijadili hapa sio ile hisia inayodumu muda mfupi baada ya mtu kukutana na tukio lisiloridhisha na kudhoofika kwa muda mfupi.

Sonona ni hali ya kihisia inayothibitika kutoka kwa mtuu fulani kukosa kabisa matumaini yoyote yale ya nafsi yake na kukosa uwezo wote wa nafsi yake kuishi matamanio ya nafsi yake. (Bibring, 1953). Hivyo kujikuta akikosa raha, akijawa na mtazamo hasi kujihusu yeye uliojawa na kujiona aliyeshindwa kwasababu ya unyonge au udhaifu aliokuwa nao. Hivyo kuishia kuona na kutilia mkazo upande wa udhaifu wake hata Kama sio udhaifu, kuona hastahili kabisa kuishi na pia kuhisi hata watu wamzungukao humuona hafai kabisa kutokana na kushindwa kuyaishi malengo ya nafsi yake ambayo binafsi huyachukulia imara, bora na yanayomstahili.

Mara nyingine sonona haieleweki kwa watu wanaowazunguka wahanga wa sonona kwani hutokea kwa kupingana na uhalisia (paradox). Kwa mfano: Hammen anasema kuwa mwanamke aliyehitaji mtoto kwa muda mrefu na baadae akafanikiwa kupata mtoto na matokeo yake anapata sonona pia kwa tukio hilo alilokuwa analihitaji maisha yake yote. Mkurugenzi wa kampuni kupatwa sonona kutokana na kupandishwa cheo hiko ambacho alikitafuta kwa udi na uvumba. Mwanamke kupata sonona baada ya kufiwa na mbwa wake wakati hakupata sonona mume wake alivyofariki. Hammen anadai bado chanzo cha ukinzani huu hakijajulikana.

Hammen anadai sonona hutawala nyanja nne yaani hisia(affective), Utambuzi(cognitive), kimwili (physical) na kitabia ( behaviour) kama inavyoelezewa hapa chini.

  1. Dalili za kuathirika kihisia. Sonona ni moja kati ya magonjwa au matatizo ambayo kwa ujumla huitwa matatizo ya kuathirika kwa hisia ( affective) yenye maana kujitokeza kwa hisia au hali isiyo ya kawaida kabisa kama njia inayotambulisha kudhoofika kwa mhanga wa tatizo hili. Hivyo Hammen anadai kuwa hali zitawalazo kwa mtu huyu ni huzuni, uchungu usioelezeka, kujihisi yupo chini sana na pia kuhisi kichwani yupo mtupu. Katika hali hii hakuna kitu kinachoweza kumpatia mtu raha au kumridhisha hata yale mambo aliyofanya zamani kama vile kazi yake, burudani, kuwasiliana na watu katika jamii yake na hata tendo la ndoa pia, ambayo yalimfurahisha na kumletea hisia chanya nayo pia humkera. Hata mahusiano yake ya muhimu kama familia yankuwa hayana maana na akifanikiwa kukamilisha jambo bado haridhiki. Kwa watu wenye sonona hii hali ya kupoteza hamu ya kufurahia maisha ni moja ya viashiria vinavyopatikana kwa watu wengi wenye tatizo hili.
  2. Dalili za Utambuzi. Baadhi ya watu wameuweka sonona kama tatizo la kufikiri Kama ilivyo tatizo la kihisia. Nadharia ya utambuzi kuelekea watu wenye sonona inalenga katika mchakato mzima wa usafirishaji wa taarifa katika ubongo wa mlengwa. Kinachotajwa kuwa ni kudumisha mawazo hasi (negative thoughts) yanayoegemea katika upande mmoja wa mambo yanayomshusha mtu au kumfadhaisha  katika mchakato huu wa taarifa ni sifa kubwa ya kudumaa kwa ufikiri katika hali hii ya sonona. Kudumaa huku huhusisha, kujumuisha taarifa kupita kiasi ( overgeneralization) na kujipa sifa hasi, zinazolenga kujishusha nafsi binafsi ya mhanga wa sonona.(Beck, 2002). Hammen anadai nadharia hii ya utambuzi inaakisi kukosekana kwa matumaini yoyote kwa uwezekano wa mhanga kuendesha matokeo anayoyatamani katika maisha yake. Ufikiri hasi unaoonesha kudumaa humsababisha mhanga kuhisi kushindwa kufanya maamuzi, kuelekeza akili yake katika mambo ya msingi kama masomo na pia kupoteza kumbukumbu.
  3. Dalili za kuathirika kitabia. Kutokana na kupoteza ushawishi katika nafsi na mazingira yamzungukayo mhanga wa sonona huacha kazi za kijamii au kupunguza utendaji kazi aliowahi ufanya mwanzo na uliowahi mletea faraja.
  4. Dalili za kimwili au kifizikia. Haya ni matokeo ya sonona yanayojitokeza katika mwili wa binadamu ambayo huwa na sifa ya kupoteza nishati kwa mhanga wa sonona, kukosa hamu ya kula na kupata shida katika usingizi. Kupoteza nishati ni dalili ambayo  wahanga wengi wa sonona hudai inawapata ambapo husababisha wajihisi uchovu uliopitiliza, kuhisi wamebeba kitu kizi sana na pia kukosa stamina au uwezo wa kuhimili kufanya kazi au kukamilisha jukumu fulani. Katika kulala mhanga anaweza kulala kupitiliza, kukosa usingizi au kuamka usiku wa manane kabla asubuhi haijawadia ( early morning awakening).












MAREJELEO.

Beck, T. ( 2002). Cognitive models of depression. Clinical Advances in Cognitive Psychotherapy: Theory and Application. Springer Publishing Company. ( P. 29-30)
                      Retrieved from;
https:// books.google.com

Bibring, E. (1953 )The Mechanism of depression. In P. Greenacre (Ed), Affective disorders; psychoanalytic contributors to their study. International Universities Press.
                     Retrieved from;
https://scholar.google.com

Depression(2017)
                    Retrieved from
https://www.who.int/westernpacific/health-topic/depression.

Hammen, C. (1997). Depression.Psychology press Ltd publishers. Uk
                     Retrieved from
https://books.google.com

Jehovah's Witness. (2017). Kushuka moyo. Amkeni. Watchtower Bible and the Tract Society of New York, Inc.(p.3)



Comments

Unknown said…
williumgeorge8@gmail.com > Greatest 🙏
Anonymous said…
Asante san blogger
Unknown said…
Sonona mbaya sana
Asante kwa ufafanuzi mzuri
Unknown said…
Sonona mbaya sana
Asante kwa ufafanuzi mzuri

Popular posts from this blog

KULALA KUPOOZA

NEUROPLASTICITY