NEUROPLASTICITY

  By Bernadether Bwire.

Hii makala imeandikwa kwa ajili ya watu wote kwa dhumuni la kujifunza jinsi ubongo wa binadamu unavyofanya kazi katika nyakati mbalimbali, kuelewa utofauti uliopo kati ya mtu na mtu na hivyo kuufurahia, kuuishi na kuukumbatia.

 Jinsi Ubongo unavyobadilika kukabiliana na Mazingira. 

Ubongo wa binadamu umejengwa/umeumbwa kwa namna ya kumwezesha aendelee kuishi/kuwepo (survive) katika nyakati ngumu au kipindi cha hatari. Lara Boyd daktari na pia mtafiti wa mambo yahusianayo na ubongo wa binadamu anasema, "binadamu pamoja na ubongo wake ulio wa plastiki hujengwa na mazingira yaliyomzunguka". Na hivyo basi ubongo unasifa ya kubadilika badilika ili kukabiliana na mazingira yamzungukayo mtu. Kila tunapojifunza kitu kipya au ujuzi mpya tunabadili ubongo wetu. Pia kila tunachokifanya, tunachokutana nacho au kukipitia hujenga ubongo wetu na hivyo inaweza kuwa Jambo jema au baya kwetu. Mabadiliko haya hayana kikomo kwani mabadiliko hayo yanatokea kwa watu wa jinsia yotote na rika zote. Ni habari njema sana kwetu sote kujua Kuna tumaini siku zote la kuwa vile unavyotaka wewe (kuenenda katika viwango vyako vya ubora), kujifunza ujuzi wowote unaoutaka, kukabili mazingira yetu yatuzungukayo na pia baada ya ubongo kujeruhiwa na kuharibika kwa baadhi ya seli za neva na hivyo kushindwa kufanya kazi fulani, ubongo kwa kupitia sehemu ya karibu ambayo haijajeruhiwa kuweza kwa mara nyingine kuzifanya kazi hizo japokuwa inaweza isiwe vizuri au kwa ubora Kama pale awali. Mabadiliko haya ya ubongo yanawezeshwa na sifa iitwayo "NEUROPLASTICITY".


Namna ambavyo ubongo unachakata taarifa fulani nakutoa majibu kuhusu taarifa hiyo unajengwa na mtu mwenyewe kutokana na hali ya mazoea aliyojijengea katika mazingira fulani. Kama namna ubongo unavyochakata taarifa hutokana na mazoea ya mtu binafsi ni dhahiri kuwa mtu huyohuyo anaweza badili ubongo wake kuenenda taarifa ileile kwa kuacha kuenenda katika mazoea aliyozoea na kuanza kujenga tabia nyingine ambayo itajenga mchakato mpya wa muundo wa ubongo. Hebu tuchunguze kwa umakini mifano ifuatayo ya miitikio tofauti tofauti ya ubongo inayojengwa na matumizi binafsi ya mtu. 

Rahma alikwenda nyumbani kwao Side na baada ya kukutana na mbwa aliyembwekea kupita kiasi Rahma aliweka akilini mwake kwamba mbwa ni adui kwake, na mara ya pili alipokutana na mbwa watatu wakitembea barabarani aliwakwepa na kupita njia nyingine na mara kwa mara alivyokutana na mbwa yoyote yule alifanya kila jitihada kumkwepa mbwa huyo. Na hivyo hii tabia ilijengeka kichwani mwake na kila Rahma akikwepa ama kukimbia mbwa hawa hujihisi amani tele moyoni wakati kila anapokutana na mbwa hujihisi mapigo ya moyo kwenda kasi, uingiwa na uwoga uliopitiliza bila kukali mbwa anayemuogopa anaweza kuwa na madhara au la.

Katika siku ya Ijumaa mida ya saa kumi na mbili na nusu jioni , tarehe mwezi wa nane mwaka 2006, akiwa na umri wa miaka sitini na sita (66) I.K ghafla alianguka kutoka katika meza aliyokuwa amekaa uso wake ukiangalia chini (aliangukia uso) . I.K hakuweza kusogeza mkono na mguu wake wa upande wa kulia na hakuweza kuita mtu aje amsaidie kutokana na tukio hilo kumfanya ashindwe kuongea. Baadae ilikuja kugundulika kwamba Kuna mshipa wa upande wa kushoto uliojeruhiwa vibaya sana na hivyo kusitisha kusambaza damu kwa nusu ya upande wa kushoto wa ubongo. I.K alipatwa na Ischemic stroke. I.K alipooza upande wa kulia wa mwili wake (hemiplegia), I.K alipoteza uwezo wa kuongea (aphasia) na kuandika ( agraphia). Lakini baada ya miaka minne kutoka kwenye tukio hilo I.K aliweza tayari kuchezea Piano kwa kutumia mkono wake wa kushoto, pia I.K aliandika vitabu, alichora picha kwa ajili ya maonesho japokuywa alishindwa bado kuongea  vizuri na kuponya kila kitu.

Fikiria pale Anna aliyeishi miaka yake ishirini ( 20 ) bila kupiga ngoma yoyote wala kuonesha dalili ya kujua kupiga ngoma miaka yote hiyo mara tu alivyofikisha miaka 22, alijifunza kupiga ngoma kwa muda wa miezi sita na akaendelea  ku fantastic mazoezi ya kupiga ngoma mara kwa mara na kujikuta akiwa mpiga ngoma mzuri sana ambaye anahudhu hiria maonesho mbalimbali kwa ajili ya kuburudisha watu kwa ngoma za asili . Na Asifiwe amejifunza kupinda vitenge kwa kutumia cherehani kwa mara ya kwanza, ambapo amefanya zoezi hilo na kulielewa kabisa kwa muda wa masaa matatu. Lakini baada ya kuja kesho yake alikuwa amesahau kila kitu alichojifunza Jana.

John, kijana aliyeogopa sana kukaa kati ya watu wengi (social anxiety) akihisi hatari kila wakati akiwa kwenye mazingira ya watu wengi ambapo mapigo yake ya moyo huenda kasi sana, hutetemeka na kuondoka sehemu hiyo akihisi kujilinda nafsi yake dhidi ya kundi kubwa la watu ambalo binafsi hulichukulia kama tishio kwake. Mara baada ya kukutana na Amina aliyemsaidia kukaa kati ya watu wengi kwa mara ya kwanza wakiwa katika kongamano la vijana na  hatimaye John kuhusu kumbe kukaa katika kundi kubwa la watu ni kawaida, na kuanza kuhudhuria katika mikutano, mihadhara na kongamano mbalimbali hatimaye John hakuhisi ile hali ya moyo kwenda mbio tena, hakuhisi kutetemeka wala kuondoka katikati ya matukio hayo yanayohusisha kikundi kikubwa cha watu.


A ni raia anayetoka nchini Ujerumani kwa jukumu la kuja kueneza dini ya kikristo nchini Tanzania, ambapo anakutana na changamoto ya lugha. Ili kueneza dini ya kikristo kwa wati wengi A ilibidi ajifunze lugha ya kiswahili ya wazawa katika umri wake huohuo ili kuendana na mazingira ya kitanzania. Baada ya kukaa muda mrefu nchini Tanzania A alijifunza kuwasiliana na wazawa kwa kutumia lugha yao ya Kiswahili.


 " NEUROPLASTICITY"

Ndani ya makala hii tutajadili hasa mabadiliko ya kimuundo ya ubongo na tutagusia kidogo mabadiliko ya kikazi yanayotokea katika ubongo.

Neuroplasticity ni uwezo wa ubongo kujibadili wenyewe ili kukabiliana na mazingira yamzungukayo mtu. Mabadiliko haya yanaweza kuwa ya kimuundo (structural plasticity) au kikazi (functional plasticity). Mabadiliko ya kimuundo hutokea pale ambapo mtu amejifunza au kuingiza uzoefu mpya katika ubongo hivyo kuanzisha mawasiliano mapya ya seli za neva na matokeo yake ni kubadilika kwa muundo wa mzunguko wa seli za neva katika ubongo ambao unatofautiana na muundo wa seli za neva wa hapo awali (Lara Boyd, daktari wa binadamu na mtafiti wa mambo ya ubongo anasema kujifunza huku kunatofautiana kati ya mtu na mtu na huwa ni wa kipekee ndiyo maana utakuta kwa mtu fulani kujifunza kucheza mpira wa miguu ni virahisi sana kwake kuliko kujifunza mpira wa tenesi wakati kwa mwingine ni kinyume). Mabadiliko ya kikazi hutokea pale ambapo sehemu ya ubongo ambayo haijajeruhiwa kuchukua na kufanya kazi zilizokuwa zikifanywa na sehemu za ubongo zilizojeruhiwa. (Mabadiliko hutofautiana baina ya mtu na mtu na kwa mujibu wa Lara Boyd, anasema kuwa baada ya wao kufanya uchunguzi waligundua Kuna upekee mkubwa sana katika mabadiliko haya na kila mtu hufanya uponyaji wa kazi kwa namna yake ya kipekee sana na ndio maana njia aliyoitumia mtu fulani kujipatia uwezo wake wa kufanya kazi unaweza usifanye kazi kwa mtu mwingine). Hii hutokea pale ambapo mtu ameumiza sehemu baadhi za ubongo wake ambazo huwa na wajibu wa kutekeleza kazi flani na hivyo kushindwa kuwajibika na hivyo mtu huyo kujifunza upya kuzifanya kazi hizo.

Emma McAdam mshauri wa mambo ya ndoa na familia anasema ubongo umeumbwa kujibadilisha wenyewe wakati wote na hubadilika kutegemea na namna unavyotumiwa na mtu binafsi. Pia anadai kuwa kubalisha mfumo wa kufikiria na kuenenda kwa mtu hubadilisha muundo wa ubongo wake. Hivyo ubongo hutusaidia kukua, kujifunza na kupona pale tunapokuwa tumejeruhiwa. Japokuwa Emma anadai uwezo mtu aupatao baada ya kujeruhiwa sehemu fulani ya ubongo wake sio kama ule uwezo aliokuwa nao hapo awali ( not perfect).

Ubongo wa binadamu ni chombo kilichoundwa na zaidi ya bilioni themanini za seli za neva (neurons), na kila seli ya neva moja inaweza kuwasiliana na seli za neva nyingine mara elfu kumi (10000). Ujuzi au uzoefu mbalimbali hutengeneza mawasiliano mbalimbali baina ya seli za neva yanayounganishwa kupitia synapses. Kwahiyo inategemea ni seli zipi za neva zimeshtuliwa au kuamshwa  na  hivyo kutumika mara nyingi kusafirisha kemikali zilezile ndizo huwa imara zaidi kuliko nyingine na hivyo kitengeneza tabia ya mtu. Pia neva za seli ambazo hazishtuliwi mara kwa mara (huwa dhaifu). Hapa hutumika ile kanuni ya kinachotumika mara kwa mara hukua na kuwa imara lakini kisichotumika huwa dhaifu  ( use it or lose it ).
Hivyo ujuzi tunaoufanya mara kwa mara (tabia)  hufanya seli za neva husika imara kuliko ujuzi tusioufanya mara kwa mara ambao hufanya seli za neva husika kuwa dhaifu.

Lara Boyd mtafiti wa mambo ya ubongo anasema kuna michakato ya aina tatu inayosababisha mabadiliko ya ubongo wetu. Ambayo ni:
  1. Kemikali
  2. Kubadilika muundo na 
  3. Kubadilika kikazi.
Katika kemikali, Lara anadai badiliko hili hudumu kwa muda mfupi na uhusisha kumbukumbu ya muda mfupi kati ya seli mbili za neva. Mfano: Kwa mara ya kwanza unajifunza kucheza bao na kuelewa sana, lakini siku inayofuata ikatokea umesahau kila kitu ni kwasababu kemikali iliachiwa kwa wingi sana ambayo haikubadili mfumo wa muundo wa ubongo hivyo kudumu kwa muda mfupi sana. Hii inaelezea hali ya Asifiwe katika mfano wetu wa awali.
    Kubadilika kimuundo kunatokana na mazoea au mazoezi (practice) ya muda mrefu katika ujuzi Fulani ambayo hutunzwa katika kumbukumbu ya muda mrefu (hippocumpus) na hivyo kubadili muundo wa ubongo. kutokana na seli mbili za neva kutoa mara kwa mara taarifa ile ile na hivyo kujenga mawasiliano imara baina ya seli za neva ambayo hubadili muundo. 

    Kubadilika kikazi hutokana na sehemu iliyokuwa ikifanya kazi awali kujeruhiwa na hivyo kushindwa kutimiza wajibu wake na matokeo yake sehemu nyingine kabisa tofauti na iliyojeruhiwa kuchukua kazi hizo na kuzifanya. Lara anadai kuwa vyote hivi vitatu huchangia kujifunza kwa mtu.


    Maguire et al. (2000) anasema kubadilika kikazi kunatokea baada ya seli za neva zilizokuwa zimelala (sababu ya kutokufanya kazi mara kwa mara) kutokana na kutokupokea taarifa zinaamshwa (activated) na kuanzisha mawasiliano yatakayo ziba pengo la sehemu ya ubongo iliyojeruhiwa. Hii huruhusu uhusiano mpya baina ya seli za neva na hivyo kuruhusu uponyaji kuendelea mahali palipo jeruhiwa.


    Lara anasisitiza kuwa nahodha wa Neuroplasticity ni tabia zetu (mazoea yetu) akimaanisha tukitaka kujua kufanya kitu fulani, tunatakiwa tukifanyie mazoezi ya mara kwa mara, hivyohivyo tukitaka kuacha mazoea fulani tunatakiwa kujizoeza kutokufanya mazoea hayo ambayo baadae itafanya mawasiliano ya seli za neva zinazohusika kwa mazoea hayo kuwa dhaifu sana. Pia tukitaka tuenende katika mwenendo fulani tunatakiwa tukifanyie mazoea ya mara kwa mara ili kuzalisha njia mpya kabisa na imara za seli za neva na hivyo kubadili muundo wa ubongo wetu. Lara anashauri kuwa tuwe waangalifu Sana na tabia tuzifanyazo kila siku kwani zinabadilisha ubongo. 

    MFANO WA NAMNA  NEUROPLASTICITY INAVYOWEZESHA MABADILIKO YA TABIA AU MWENENDO WA MTU ALIYEKUWA NA MARADHI YA WASIWASI. 

    McAdam katika mfululizo wake wa "THERAPY IN A NUTSHELL", anasema kuwa tukielewa namna ubongo unavyochakata taarifa ya wasiwasi uliopitiliza itatusaidia kudhibiti au kukabiliana na hali hii. Emma anajadili mzunguko wa wasiwasi au mzunguko unaojenga mazingira ya wasiwasi uliozidi najinsi ya kuukabili. Alihainisha vitu vinne vinavyojenga mazingira haya ambavyo ni:

    1. Kutafsiri hali fulani kama tishio au hatari. Kutafsiri hali fulani kama hatari au tishio kwa mtu binafsi na yeye kuhisi ni ukweli moja kwa moja kwamba hali hiyo inaashiria hatari kwake. Mfano: Baada ya Asifiwe kutoa maoni yake darasani na Detha kuyapinga kwa kuleta hoja zake tofauti na Asifiwe, matokeo yake Asifiwe anamchukulia Detha Kama tishio kwake (au mtu yoyote anayepingana na hoja zake Kama tishio kwake)
    2. Kuepuka hali hiyo. Hivyo ili kujilinda na nafsi yake Asifiwe anaamua kuepuka majadiliano hayo ambayo anayachukulia Kama tishio kwake yeye.
    3. Kupata ahueni. Baada ya kukimbia ama kuepuka majadiliano hayo Asifiwe anajihisi kupata ahueni, kuwa huru na kupata amani. Hivyo katika hatua hii Ubongo wa Asifiwe unachakata taarifa hiyo na kuazimia kabisa kwamba "nimekabiliana na hali ile kwasababu nimeiepuka". Hivyo hali Kama hiyo ikijirudia tena na tena Asifiwe anakimbia majadiliano kwa kujua kwamba ndio njia pekee ya kukabiliana au kuishinda hali hiyo.
    4. Hivyo ubongo unazalisha kemikali za wasiwasi kwa wingi kila wakati Asifiwe anapokutana na hali hiyo hivyo kusababisha tabia kwa Asifiwe inayompelekea kukwepa au kukimbia majadiliano kila wakati anapokutana nayo.
    Emma anashauri kuwa tunatakiwa tuelewe kwanza wasiwasi ni nini, na kazi ya wasiwasi katika maisha ya binadamu, pia tujue kutofautisha wasiwasi na maradhi ya wasiwasi ambayo yanatokana na tatizo la akili kutafsiri hatari pasipokuwa na hatari ( anxiety disorders). Emma anasisitiza kuwa wasiwasi sio kitu au hali mbaya na ipo kumfanya mtu asiwe huru tu (uncomfortable) ili kumuepusha na hali halisi ya hatari. Mfano: Baada ya kubakiza wiki moja tu ili kufanya mtihani wa taifa, Asifiwe anapatwa na hofu kubwa Sana au wasiwasi ambao unaomfanya azidi kusoma Sana ili kuepuka kufeli mtihani wake. Hivyo basi wasiwasi ulimfanya Asifiwe asiwe huru na akose Raha ili afanye kitu ambacho no sahihi na ni kusoma ili afaulu mitihani yake na hivyo kuepuka hatari halisi iliyokuwepo mbele ya Asifiwe nayo ni kufeli mitihani yake ya mwisho. Hivyo badala ya kuchukulia wasiwasi kama hali mbaya ama tishio tunaweza kubadili mtazamo huu unaojenga tabia isiyofaa kwetu.

    Pia Emma anashauri kuuvunja mzunguko wa wasiwasi kwa kuacha kukimbia au kukwepa hali tunazohisi ni tishio kwetu. Mfano: Baada ya Asifiwe kukaa kwenye majadiliano na watu na kutetea hoja zake dhidi ya hoja za Detha ubongo wake unazalisha kitu kipya kwamba hoja zinazopinga hoja zake sio tishio bali zipo ili kuimarisha majadiliano kwa ujumla na pale ambapo Asifiwe atarudia kutetea hoja zake mara kwa mara dhidi ya mawazo yaliyo kinyume na yeye,ubongo wake utabadili kabisa mzunguko wa seli za neva husika na kufanya mzunguko wa awali kuwa dhaifu.

    Hivyo basi tukielewa mabadiliko ya ubongo wetu na namna tunavyouchochea kupokea na kutafsiri taarifa, tutakuwa na uwezo mkubwa sana wa kubadili mitazamo yetu juu ya maisha na watu watuzungukao, pia tutakuwa na uwezo wa kuyaacha mambo yote yasiyo salama kwa nafsi zetu na kujizoeza kufanya mambo yaliyosalama kwa afya na nafsi zetu. Bila kusahau kuelewa utofauti uliopo kati ya mtu na mtu katika kitendo cha kujifunza, na hii inaelezea dhana ya mtu mmoja kujifunza somo la hisabati kwa urahisi sana na kwa muda mfupi kuliko mtu mwingine wakati huyu mtu mwingine anauwezo wa kujifunza masomo ya sanaa kwa urahisi zaidi kuliko huyo wa kwanza. Hivyo tunashauriwa kujifunza zaidi vitu ambavyo ni rahisi kwetu na vinatakiwa kwa ubongo wetu.








    MAREJELEO.

    After watching this, your brain will not be the sama /Lara Boyd/ TEDxVouver
    https://youtu.be/LNHBMFCzznE.

    Dr. Lara Boyd: Plasticity and the Brains of Children Learning Disabilities.
    https://youtu.be/AMINf3Dt91M.

    Neuroplasticity and the power of the brain- Magical mind-HD Documentary
    https://youtu.be/85UaAR-ZPzU.

    Rewiring the Anxiety Brain-Neuroplasticity and the Anxiety Cycle (Anxiety skills#21)
    https://www.udemy.com/change-your-brain/?couponCode =THERAPYNUT.



                 



    Comments

    Anonymous said…
    Nmejifunza mengi sana ndani ya hii post
    Unknown said…
    Unatufunguli dunia

    https://reprogrammingourminds.blogspot.com/2019/12/neuroplasticity.html
    KiseKazamwendo said…
    Nimejifunza mengi kutokana na post hii.asante Sana
    Bernadether said…
    Thanx to u all for your huge support...Let's wait for more articles
    Unknown said…
    Waoo nimejifunzaaa kituu aiseeeee hongeraa

    Lida said…
    Woow.
    Sure.
    Thanks
    Lida said…
    Woow.
    Sure.
    Thanks

    Popular posts from this blog

    KULALA KUPOOZA

    SONONA/KUSHUKA MOYO